Ajibu, Chirwa wasajiliwa


By THOMAS NG’ITU
KIWANGO kibovu cha mastraika; Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa, kimewafanya mabosi wa klabu hiyo waanze kufikiria kuingia sokoni upya ili kufanya usajili wa maana katika idara ya ushambuliaji.
Mabosi wa kikosi hicho wameanza kuwapigia hesabu za haraka wachezaji watatu, Adam Salamba wa Lipuli na Marcel Boniventure wa Majimaji na straika Mnigeria, ili waweze kuongeza nguvu kwa msimu ujao baada ya kuona viwango vya Ajibu na Chirwa vimeshuka kwa sasa.
Pamoja na kuwa Yanga imekuwa ikiwakosa mastraika wake matata; Donald Ngoma na Amis Tambwe ambao walifunga mabao zaidi ya 45 katika mashindano yote msimu wa 2015/16, matumaini makubwa yalikuwa kwa Ajibu na Chirwa ambao sasa viwango vyao vimeanza kutia shaka.
Ngoma na Tambwe wamekuwa wanasumbuliwa na majeraha ya muda mrefu hivyo, kuifanya timu hiyo kuwategemea zaidi mastaa hao wawili.
Ajibu na Chirwa walianza vizuri msimu kwa kufunga mabao 11 katika mechi saba tu za mwanzoni msimu huu, lakini tangu mwaka ulipobadilika viwango vyao vimeshuka na kuigharimu timu hiyo ambayo imecheza mechi nane mfululizo sasa bila kuonja ushindi.
Tangu mwaka huu umeanza, Ajibu na Chirwa, wameifungia timu hiyo mabao tisa tu katika mashindano yote ambayo timu hiyo imecheza ikiwa ni kiwango kibovu zaidi kuwahi kuwakumba mastraika wa mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara.
Mbali ya Kombe la Mapinduzi, Yanga imecheza mechi 13 za Ligi Kuu na saba za mashindano ya kimataifa katika kipindi hicho huku Ajibu akichemsha zaidi kwa kufunga mara mbili tu katika michezo hiyo.
Pamoja na Chirwa kufunga mabao saba, matatu kati ya hayo alifunga kwenye mchezo mmoja dhidi ya Njombe Mji, hivyo amecheza mechi zaidi ya 15 ambazo hakuweza kufunga bao jambo ambalo sasa limeirudisha Yanga nyuma.
Hali ni mbaya zaidi katika mashindano ya kimataifa ambapo Yanga imecheza michezo saba mpaka sasa, lakini Ajibu na Chirwa wamefunga mabao mawili tu, hivyo kudhihirisha uwezo wao huenda ni wa kuzifunga timu dhaifu kama Njombe Mji na Mbeya City tu.
Ajibu aliifungia Yanga bao moja la ushindi dhidi ya St. Louis mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa wakati huo huo Chirwa naye aliifungia Yanga bao la kufutia machozi walipofungwa 2-1 na Township Rollers.
WADAU WAFUNGUKA
Straika wa zamani wa Yanga, Henry Morris, ambaye kitaaluma ni kocha, amesema wachezaji hao wanavyopunguza kasi yao ya ufungaji, lazima benchi la ufundi pamoja na mabosi wajiulize tatizo lipo wapi kabla hawajaanza kuwazungumzia vibaya.
“Unajua mtu kama una matatizo ya familia ni ngumu kufanya vizuri, akili inakuwa na mambo mengi kichwani, viongozi wanabidi wajue hilo. Lakini, inawezekana kuna mazoezi ambayo walikuwa wanayapata awali na sasa hawayapati. Kikubwa ni benchi la ufundi na mabosi kuwa karibu na wachezaji wao,” alisema. Akizungumzia usajili mpya, Morris alitoa angalizo: “Mchezaji unayemsajili kwa kufanya vizuri mechi mbili atakupoteza, wanatakiwa wasajili mchezaji ambaye anaonekana ni mpambanaji, wachezaji wetu wa kibongo wanapokwenda Simba na Yanga hujikuta wanashindwa kufanya vizuri.”
Naye mchambuzi wa kituo cha Azam TV, Ally Mayai, alisema Ajibu na Chirwa wanalazimishwa kucheza nafasi ambazo si zao hivyo, wanajikuta wanapewa majukumu kutokana na matatizo ya majeruhi.
“Chirwa na Ajibu si washambuliaji, wale ni viungo wa pembeni lakini wamejikuta wakipewa majukumu mapya kutokana na kukosekana mtu sahihi. Sidhani kama Tambwe na Ngoma wangekuwepo wangecheza kwenye nafasi hizo,” alisema Mayay, ambaye anatajwa kuwa ndiye mchambuzi mahiri zaidi nchini kwa sasa.


Share on Google Plus

About Chagaboy

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment