Mwadui yaapa kuijeruhi Yanga


By Saddam Sadick
Mwanza. Wakati Mwadui FC ikitarajia kuwakabili Yanga kesho Jumamosi mjini Shinyanga, kocha wa timu hiyo, Ally Bizimungu amewapiga mkwara wana Jangwani hao kuwa lazima wachezee kichapo.
Mpambano huo unatarajiwa kupigwa kwenye uwanja wa Kambarage, ambapo Yanga itaingia uwanjani ikiwa na rekodi ya kutopata ushindi kwa mechi nane mfululizo katika mashindano yake.
Hadi sasa Yanga imevuna pointi 48 ikiwa nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 26, huku Mwadui wakishika nafasi ya 12 kwa alama 30 baada ya kushuka uwanjani mara 27.
Kocha Bizimungu alisema kuwa mchezo huo ni muhimu kwao katika vita ya kusaka pointi tatu ili kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Alisema kuwa anaamini wapinzani wao wamekuja kwa tahadhari kubwa ya kusaka ushindi, lakini hawatakubali timu hiyo ifufukie kwao na kwamba lazima washinde.
“Ni mchezo mgumu lakini muhimu sana kwetu, hatutakubali wafufukie kwetu,kwa sababu tumeangalia mechi zao za viporo Yanga haijashinda kwa hiyo hata kwetu kesho lazima wafe tu,” alisema Bizimungu.
Aliongeza kuwa katika kikosi chake ni mchezaji mmoja, Evalist Mujwahuki ambaye hatacheza kutokana na tatizo la misuli na kwamba amemwandaa mbadala wake.
“Katika mechi tatu zilizobaki tunahitaji ushindi mfululizo ili kutimiza malengo yetu ya kumaliza Ligi tukiwa nafasi saba za juu, hivyo kila mchezo una umuhimu sana kwetu,” alisema Kocha huyo.


Share on Google Plus

About Chagaboy

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment